Kampeni ya ONDOA CCM DAR kuendelea leo 11/02/2012

Ndugu wananchi ratiba ya ONDOA CCM DAR: KESHO JMOS. JIMBO LA KAWE MAENEO YA TEGETA, JIMBO LA KINONDONI MAENEO YA SUNNA NA JIMBO LA TEMEKE MTONI KWA AZIZI ALLY UTAONA BENDERA BARABARANI ZITAKUPELEKA MPAKA KWENYE MKUTANO.

ILA POLICE WALITAKA KULETA HILA JUU YA MKUTANO WA TEGETA KWA KUTUANDIKIA BARUA YA KUAHIRISHA MKUTANO WETU KWA HOJA YA MASHAMBULIO YA KIGAIDI, ILA NIKAONGEA NA RPC WA KINONDONI BWANA KENYELA NA KISHA TUKAFIKIA MUAFAKA AKATUPATIA KIBALI NA KUFUTA ILE BARUA YAO YA AWALI AMABAYO ILITOKEA KWENYE KITUO KIDOGO CHA KAWE.

WATATUUA KWA RISASI ZA MOTO, WATAKUFA KWA PRESHA YA DHAMBI, AHSANTENI MUNGU YUPO UPANDE WETU NA MSIOGOPE.

HENRY J KILEWO

KATIBU (M) KINONDONI

KANDA YA DAR ES SALAAM

 

kamanda Kilewo akifungua msingi wa chama jimbo la Kawe

Katibu wa chadema mkoa wa kinondoni na Kanda Maalum ya Dar es salaam Bwana Henry Kilewo akifungua msingi wa chama, kamanda aliwatia ujasiri vijana akiwataka kujiandaa kupambana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha, na kutaka wasiongope kufa wakipigania ukweli. kamanda aliendelea kusema Watatuua kwa risasi za moto na wao watakufa kwa presha za dhambi tusiongope mapambana lazima yaendelee… huyo ni kamanda Kilewo, kisha akatuaga na kuelekea Arusha.

KWA NINI SIKUMSALIMIA JK,DK.SLAA

Fredy Azzah
KATIBU Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa  amesema kuwa, hakuweza kusalimiana na Rais Jakaya Kikwete kutokana na Jiografia ya eneo la makaburini lilivyopangwa na watu wa usalama wa taifa pamoja na kamati ya mazishi kutomruhusu kufanya hivyo.

Hata hivyo Dk Slaa alisisitiza kuwa, kwa upande wake, kwenye msiba siyo sehemu ya kwenda kwa ajili ya kusalimiana na watu ama kurekebisha mambo yaliyoharibika bali ni sehemu ya kumwombea marehemu.

“Siyo hulka ya Dk Slaa kutumia misiba kama sehemu ya kusalimiana, wala kutengeza mambo yaliyoharibika, mimi huwa naenda kwenye msiba kwa lengo moja tu la kumwombea marehemu, huwa simtazami hata mtu aliyekaa pembeni yangu,” alisema Dk Slaa alipozungumza kwa njia ya simu  jana.

Alifafanua kuwa, katika eneo la makaburi kulikuwa na mabanda matano ambayo yalipangwa kwa ajili ya Askofu, Rais, Viongozi wa vyama vya siasa, mwili wa marehemu  na familia na banda jingine lilikuwa la watu wengine waliohudhuria mazishi hayo.

“Sasa kutoka alipokuwa amekaa Rais mpaka kwenye banda nilipokuwa mimi, kulikuwa na umbali wa karibu  mita 20, sasa mlitaka nikimbie kumsalimia Rais nivunje protokali kisha nikamatwe na usalama wa taifa,” alisema Dk Slaa. Alisema alikuwa mtu wa kwanza kufika makaburini kwa lengo la kuangalia jinsi kaburi la mbunge wa chama chake lilivyochimbwa kisha akaonyeshwa sehemu ya kukaa na watu wa usalama wa taifa.

Alisema kuwa, hata katika wakati wa kuaga mwili wa Marehemu Regia Mtema, katika ukumbi wa Karejee, kulikuwa na utaratibu kama huo ambapo ilitengwa sehemu ya kukaa Makamu wa Rais, Spika wa Bunge, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani na Makamu wake na yeye Dk Slaa akawekewa sehemu yake kama Katibu wa Chama alichokuwa akikitumika marehemu.

“Mimi sipendi kuweka siasa kwenye mambo kama ya msiba, Dk Slaa siyo kichaa siyo kichaa aanze kukimbia kumsalimia Rais. Katika sehemu kama ile Rais huwa anakuja baada ya watu wote wakiwa wameshakaa, yeye ndiye hupita na kuanza kusalimia watu na hamjaona hata sehemu moja aliponyoosha mkono kunisalimia nikamkwepa,” alisema Dk Slaa:

“Msiba siyo mahali pa kutengeza urafiki, au kutengeza mambo yaliyo haribika, pale ni ibada tu na kumuombea marehemu siyo sehemu ya kufanya siasa” alisisitiza Dk Slaa. Jana baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa, Dk Slaa alishindwa kusalimiana na Rais Jakaya Kikwete katika mazishi ya Regia Mtema yaliyofanyika kijijini kwao Ipangalala Morogoro juzi.Regia alifariki dunia Januari 14 kwa ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Ruvu mkoani Pwani.  Chanzo: gazeti Mwananchi.

DK.SLAA AMPIGA CHENGA JK MSIBANI(GAZETI MWANANCHI)

AKWEPA KUKAA JUKWAA KUU, WENGI WAMZIKA REGIA
Juma Mtanda na Shakila Nyerere, Ifakara
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willbrod Slaa, jana alimkwepa tena Rais Jakaya Kikwete safari hii ikiwa katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya chama hicho, Regia Mtema yaliyofanyika katika Kijiji cha Lipangalala.Tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010, ambao Dk Slaa alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 2,271,941 sawa na asilimia  26.34 akiwa nyuma ya Rais Kikwete aliyepata kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17, Dk Slaa hakuwahi kukutana na mkuu huyo wa nchi ana kwa ana.

Katika hafla ya kutangazwa matokeo ya urais iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kwenye Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, Dk Slaa hakuhudhuria tofauti na ilivyokuwa kwa waliokuwa wagombea wenzake wote.

Jana, Dk Slaa tofauti na viongozi wenzake wa Chadema akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, hakutaka kujiweka katika mazingira ambayo yangemkutanisha na Rais Kikwete katika mazishi hayo.
Nyumba kulikofanyika shughuli za awali za mazishi, waandalizi waliandaa majukwaa mawili, moja maalum kwa ajili ya wabunge huku jingine likiwa ni maalumu kwa ajili ya viongozi wakuu ambalo alikaa Mbowe, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe.

Mbali ya kukaa viongozi hao, kulikuwa na nafasi ambayo ilikuwa imetengwa maalumu kwa ajili ya Rais. Mbali ya nafasi hiyo, pia kulikuwa na kiti ambacho ilitegemewa kwamba Dk Slaa angekalia.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo wa Chadema alikikwepa na kwenda kujichanganya katika jukwaa la wabunge na kiti hicho kubaki bila ya kuwa na mtu.

Hata hivyo, Rais Kikwete hakuweza kufika nyumbani hadi mwili wa marehemu Regia ulipopelekwa katika Viwanya vya Viungani ambako uliagwa na mamia ya waombolezaji.

Uwanjani hapo nako kulikuwa na majukwaa mawili. Kama ilivyokuwa nyumbani, jukwaa moja lilikuwa la wabunge na jingine la viongozi wa ngazi za juu lakini bado, Dk Slaa alilikwepa jukwaa hilo ambalo Rais alitarajiwa kuwa angefikia. Rais hakuweza kufika Viungani pia.

Rais Jakaya Kikwete akiweka udongo kwenye kaburi la aliyekuwa mbunge wa viti maalum (Chadema) Regia Mtema wakati wa mazishi yaliyofanyika kwenye makaburi ya Ipangalala Ifakara mkoani Morogoro jana.Picha na Juma Mtanda

Baadaye wakiwa eneo la mazishi, Rais Kikwete alifika na kushiriki tukio hilo na kisha kusalimiana na wabunge mbalimbali na viongozi waliokuwa wamefika akiwemo Mbowe, Mbunge wa Rombo Joseph Selasini, Zitto na viongozi wengine lakini Dk Slaa hakuonekana.

Ilitegemewa kuwa tukio hilo la msiba lingewaleta wanasiasa hao lakini hadi Rais Kikwete alipoondoka hakuna mahali ambako walisalimiana.
Mbali ya tukio hilo, hata katika hafla mbalimbali ambazo viongozi wa Chadema wamekuwa wakialikwa ikiwemo Ikulu, Dk Slaa hakuwahi kuhudhuria.

Novemba mwaka jana viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe, walifanya mazungumzo na Rais Kikwete, Ikulu ya Dar es Salaam kujadili suala la Katiba Mpya, lakini Dk Slaa hakuhudhuria.

Chadema wahaha
Wakati viongozi wa Chadema wakihaha kumaliza mgogoro ndani ya chama hicho wilayani Kilombero, Pacha wa marehemu Regia, Remigia Mtema amesema ndugu yake Regia alikuwa akipeleka malalamiko kwa Dk Slaa mara kadhaa kuomba asuluhishe bila mafanikio.

Hata hivyo, Remigia alisema marehemu Regia alikuwa amepanga kuonana tena na Dk Slaa katika siku za hivi karibuni kumweleza kinachoendelea.

Akizungumzia suala hilo, Dk Slaa alisema alishaanza kushughulikia mgogoro huo lakini msiba huo ndiyo uliomkwamisha.

“Ni kweli nimekuwa nikielezwa tatizo hilo na tayari nilishaanza kulifanyika kazi ila sasa siwezi kusema suala hilo limefikia wapi kwani wote tuko kwenye mazishi,” alisema.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wabunge wa Chadema waliotangulia kufika katika msiba huo, Mchungaji Peter Msigwa, Ezekia Wenje na Lucy Owenya, walikutana na uongozi wa kata wa Chadema ili kumaliza mgogoro huo.

Katibu mwenezi wa Chadema kata ya Ifakara, Antony Kamonalelo alisema viongozi hao walikaa na wanachama hao na kuwataka wapunguze munkari ili kumruhusu Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kilombero, Salum Ngozi na Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Kiwanga kuhudhuria mazishi.

Hata hivyo, inadaiwa kwamba wanachama hao waliukubalia uongozi huo kumruhusu Susan peke yake kuhudhuria mazishi hayo.

Juzi, wanachama hao walimtimua msibani Ngozi kiasi cha kuwalazimu polisi waliokuwa eneo hilo kuingilia kati kwa kumchukua mwenyekiti huyo na kumpeleka katika Kituo cha Polisi Wilaya.

Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Ngozi kutimuliwa katika msiba huo. Mara ya kwanza ilikuwa siku moja iliyotangulia ambayo ilimlazimu Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Francis Miti kuingilia kati.

Ngozi amekuwa akidai kwamba anafanyiwa fujo na kikundi cha watu aliowaita wahuni na kwamba amefungua kesi ya kufanyiwa vurugu katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Kilombero na kwamba baada ya kumalizika kwa mazishi. www.mwananchi.co.tz