Waraka mahususi kwa viongozi wa dini wa Tanzania

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Salaam za X-Mas na Mwaka Mpya za Mchungaji Peter Msigwa,
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema)
Waraka mahususi kwa viongozi wa dini wa Tanzania:

kuweni macho na wanasiasa wenzangu.

 

Utangulizi
Ndugu Wanahabari,
Kwa nafasi yangu kama raia, Mbunge ninayewakilisha wananchi wa Jimbo la Iringa Mjini na Watanzania wote kwa ujumla na mmoja wa viongozi wa dini/dhehebu nchini, naomba kutumia fursa yenu na ya vyombo vyenu vya habari kutoa ujumbe mahususi kwa viongozi wenzangu wa kidini kwa manufaa ya taifa letu.
Ninapowasilisha salaam zangu hizi za X-Mas na Mwaka mpya wa 2012, ningependa kusisitiza yafuatayo kwa viongozi wenzangu wa dini, kuhusiana na nini hasa unapaswa kuwa wajibu wetu kuhusiana na mwenendo wa viongozi wetu wa kisiasa (mimi pia nikiwa mmoja wao);
 • Nianze kwa, kuwapongeza viongozi wenzangu wote wa dini waliojitokeza hadharani au kupitia vyombo vya habari hivi karibuni kupinga kusudio au mpango wa kuongeza posho za vikao kwa wabunge. Suala la malipo ya posho za vikao (Sitting allowance) kwa wabunge na watumishi wa umma pamoja na mpango wa kuongeza posho hizo kutoka sh 70,000 hadi sh 200,000 (kwa siku ya kikao), kama ulivyotangazwa na Mhe. Spika wa Bunge, Anne Makinda, hivi karibuni, limegusa hisia za Watanzania wengi wakiwemo viongozi wenzangu wa dini ambao naungana nao kuzipinga nikisisitiza msimamo wa siku nyingi wa chama chetu (Chadema).
 • Pongezi hizi zinazingatia ukweli kuwa katika suala hili la posho,Baadhi ya viongozi wa dini wameweza kuchukua wajibu wao kikamilifu wa kuwa juu ya wanasiasa wenye malengo mabaya tofauti na desturi iliyoanza kujengeka hivi karibuni ya baadhi ya wanasiasa hususan wale wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupenda kuwatumia vibaya baadhi ya viongozi wa dini na nyumba za ibada kama sabuni ya kujisafishia uchafu wao na ngazi ya kufikia malengo ya kuutafuta urais au ubunge na udiwani (uongozi mchafu). Ingawa kanisa ni mahali pa kusafishwa uchafu na kila mtu anakaribishwa, lakini tumkumbuke yule Simon Mchawi katika kitabu cha matendo ya mitume,aliyejaribu kununua kipawa cha Roho mtakatifukwa faida yake binafsi,Ndipo mtumishi wa Mungu Petro alipomwambia apotelee mbali pamoja na pesa yake.
 • Nawasihi viongozi wa dini wenzangu kwamba kamwe tusikubali kuwa mawakala wa kufanikisha mbio za urais mchafu. Tusikubali kuwa chini ya wanasiasa maana jukumu letu la kuwanusuru wanadamu kiroho kwa kuwaongoza kumcha Mungu, ni jukumu zito na kubwa kuliko uroho wa madaraka unaowakimbiza baadhi ya wanasiasa kwenye nyumba za ibada.
 • Ni udhalilishaji mkubwa wa huduma ya kiroho pale viongozi wa dini tunapowakaribisha wanasiasa kufanya shughuli kama za uzinduzi wa makanisa au albamu za nyimbo za kidini kana kwamba wao ndio wenye upako, utukufu na mamlaka zaidi ya kubariki kinachozinduliwa kuliko sisi viongozi wa dini wenyewe.
 • Tabia kama hii ya kuwatanguliza mbele wanasiasa kwenye shughuli za kiroho badala ya kuacha huduma hii ijitegemee yenyewe (maana Mungu ni Mkuu na mwenye uwezo kuliko siasa), kwa namna moja au nyingine imekuwa ndio kichocheo cha kufanya wanasiasa kutafuta pesa kwa gharama yoyote, ilimradi wakiitwa kwenye mialiko hiyo waweze kutoa fungu kubwa wakiamini itawajenga kisiasa hata kama hawana nia ya kweli na Mungu.
 • Tusikubali kamwe kutumiwa vibaya na wanasiasa wanaojipenyeza kwenye matukio mbalimbali kama ya harambee na uzinduzi wa albamu za nyimbo za kiinjili, kwa lengo la kujitangaza, kujisafisha na kujipendekeza kwa umma uliowakataa au kukosa imani nao.
 • Tusikubali nyumba takatifu za ibada zigeuzwe viwanja vya kampeni za kisiasa na wala tusiwe chanzo cha kuiingiza nchi yetu katika mgawanyiko na machafuko ya kidini kwasababu tu ya kuwabeba baadhi ya wanasiasa ambao ama kwa sababu ya uchafu wao au umma kukosa imani nao, wameona hawawezi tena kuwa na uhalali wa kujitangaza wala kujijenga tena kwenye majukwaa ya kisiasa bila kwanza kukimbilia makanisani. Binafsi naamini, mwanasiasa msafi anayejiamini na anayemcha Mungu kwelikweli haitaji harambee au tukio lolote la kujinadi kanisani , maana huko si pahali pake.
 • Najua kuwa Watanzania wengi wanakerwa na tabia ya baadhi ya sisi viongozi wa dini kama maaskofu, wachungaji na mapadri kubabaikia wanasiasa kwa kiasi cha kuonekana wanaidhalilisha huduma hii kuu. Kanisa likitakiwa kuzinduliwa – mwanasiasa, uzinduzi wa nyimbo ya injili – mwanasiasa, ununuzi wa magitaa – mwanasiasa, ununuzi wa maspika – mwanasiasa. Hivi hawa wanasiasa wana upako gani kana kwamba kazi ya Mungu haiwezi kufanyika bila wao?
 • Tunapokwenda kusherehekea siku kuu hii ya X Mas na Mwaka Mpya, ninawasihi tena viongozi wenzangu wa kidini, kwamba tumkumbuke nabii Baalam ambaye vitabu vitakatifu vinaeleza jinsi alivyoifanyia biashara huduma yake ya kinabii mpaka alisababisha Punda aongee;
  Tumkumbuke mtumishi wa nabii Elisha, aliyeitwa Gehazi, ambaye vitabu vitakatifu vinatufundisha kwamba alipenda pesa na zawadi akasahau mwito wake wa kitume mpaka ukoma wa Nahaman ukahamia mwilini mwake;
  Tumkumbuke Esau aliyeuza haki ya uzaliwa wake wa kwanza kwa njaa ya muda mfupi (dengu,mlo moja tu);
  Na tumkumbuke Yuda Eskarioti ambaye alimuuza mwokozi wetu, Yesu Kiristu, kwa vipande thelathini vya fedha, na kwa hiyo, sisi viongozi wa dini tusikubali kamwe kuwauza Watanzania wenzetu kwa pesa za wanasiasa wachafu.
 • Nasisitiza tena, kwamba sisi viongozi wa dini tunapaswa kuwa viongozi na sio wafuasi wa wanasiasa, tunapaswa kuwaonyesha njia wanadamu wote wakiwemo wanasiasa na sio wanasiasa watuonyeshe njia sisi, maana kufanya hivyo ni kulishusha thamani neno la Mungu.
 • Naamini kama taifa kwa ujumla tuna hali za duni za kimaisha zinazotugusa pia sisi viongozi wa kiroho, lakini hii isisababishe tukasahau misingi yetu ya kitume kana kwamba Mungu aliyetuita ametuacha. Naamini sisi viongozi wa dini tukisimama imara bila kuyumba, Tanzania yetu inayougua umaskini, ujinga, maradhi na ufisadi, hatimaye itaponywa. Hizi ndio salamu zangu za mwaka mpya kwa viongozi wa dini ambao naamini kupitia wao Watanzania wote wataongozwa vema

  Nawatakia kheri na fanaka ya X- Mas na Mwaka Mpya.
Mungu ibariki Tanzania,

 

Mhe. Godbless Lema aipongeza NCCR kwa maamuzi waliyochukua dhidi ya David Kafulila ya kumvua uanachama

“Nimesoma taarifa mbali mbali juu ya kufukuzwa uanachama kwa Mbunge  David  Kafulila na nilipata fursa  ya kutoa maoni yangu pale vyombo vya habari vilipotaka hivyo kutoka kwangu, nimefuatilia kwa makini sana mijadala mbali mbali haswa katika mtandao wa Jamii Forum na kuona mawazo ya  Watanzania mbali mbali juu ya jambo hili .Na ninafikiri ninao wajibu  kama kijana tena Mbunge kutoa maoni yangu na mtazamo wangu kwa kina juu ya jambo hili ambalo limemkuta Mbunge mwenzetu na rafiki yetu kijana Bwana David Kafulila. “ Kwanza kabisa Bwana David Kafulila pole sana lakini kikubwa zaidi jipe moyo kwani changamoto katika siasa mara nyingi ni matukio yasio ya kawaida ambayo yanaweza kushusha heshima ya mtu au kupandisha heshima ya mtu, lakini tambua kuwa matatizo sio msingi mkuu wa kuharibu ndoto ya mtu makini aliyekusudia kutimiza jambo ambalo wajibu wake ni upendo , utu na ukweli katika jamii ni imani yangu kuwa  changamoto hii inaweza kukufanya uwe kijana mwenye  hekima zaidi  kwani katika kila changamoto kubwa Duniani hapo ndipo ukombozi ulipotokea Duniani .

 Ninatambua wakati unaopitia kwa sasa wewe na familia yako na wapiga kura wako , lakini kwa mtu makini kama mimi ni lazima pia nikipongeze Chama chako kwa uamuzi wake dhidi yako , chama chako cha NCCR-Mageuzi  kimechukua hatua muhimu katika maisha yake ya siasa na kwamba  “ Nidhamu katika Chama itakuwa ni msingi mkuu katika kutafuta ukombozi wa kweli katika Taifa,  Binafsi  sifurahi wewe kufukuzwa katika Chama lakini nimefarijika na jinsi Chama  kinachukuwa  taratibu kama NCCR kinavyoweza kuchukua maamuzi magumu ya kulinda nidhamu na heshima ndani ya Taasisi ya Chama cha Siasa, Watu wengi hata mimi ningependa usamehewe , lakini David katika maisha ya siasa na Nyanja nyingine , uvumilivu na nidhamu katika kufanikisha maono au ndoto ni vitu ambayo ni msingi mkuu wa mafanikio  na hauwezi kuviepuka  ndio maana , Mtu mmoja mwenye hekima aliwahi kupata kunena kuwa “ huwezi kupata kifaranga cha kuku kwa kuvunja yai bali kwa kusubiri yai liatamiwe kwa siku kadhaa na  baadae vifaranga watatotolewa ,

Lakini vile vile Mtu huyu mwenye hekima akasema tena  “ haijalishi  unampenda mke wako kiasi gani , kuna vitu unaweza kumsaidia na kuna vitu huwezi kumsaidia “ kwa mfano huwezi kumsaidia mke wako kubeba mimba hata kama unampenda  sana , hivyo malengo makubwa katika siasa ni jambo muhimu kwa kijana makini kama wewe kufikiria lakini uvumilivu na kusubiri ni muhimu katika kufikia malengo makuu , Mimi binafsi ninatofautiana na watu wengi kwamba kupoteza jimbo ni jambo gumu na baya , hapana kupoteza jimbo kwa sababu ya kulinda nidhamu ni jambo jema linalopaswa kufanyiwa hata sherehe , hivi kweli tunaweza kupima nidhamu  na ni kitu gani katika maisha ya mwanadamu  ? na vile vile tufikirie kama leo Mbunge au Diwani akifukuzwa kwa utovu wa nidhamu na sisi tukafikiri ni makosa , je ni halali sasa vyama vya upinzani kutafuta kuunda dola kama vitashindwa kusimamia tu  nidhamu ndani ya vyama vyao  ,je vitaweza kweli kusimamia nidhamu ya dola pindi vitakapochukua madaraka ?

NCCR Mageuzi wamefanya maamuzi ya msingi na ya uhakika kulinda nidhamu ndani ya chama ambaye yeyoye atakayethubutu kulaani basi ajiulize swali hili ? Kama nafasi ya Ubunge inathamani kubwa kuliko nidhamu ndani ya chama na jamii , je mtakuwa na ujasiri kweli wa kupinga dhambi  dhidi ya utu wa mwanadamu ambapo hivi karibuni mlipewa masharti ya ndoa ya jinsia moja kama mnataka misaada ?  sasa mkisema nidhamu ipuuzwe dhidi ya nafasi moja ya Ubunge , mtawezaje sasa kuvumilia  njaa ,mateso na dhiki dhidi ya kutetea utu wenu ? nina wasi wasi kuwa  siku moja pengine mtakubali yale mashariti mliyopewa  na  waziri Mkuu wa Uingereza ili muweze  kula lakini  kwa kudhalilisha utu wenu , kwani nafasi ya nidhamu katika maisha ya binadamu haupaswi kupigiwa kura .

Hivyo tukifahamu msingi mkuu wa mafanikio  kuwa ni  pamoja na  nidhamu ya kweli , nafikiri maoni ya wachangiaji  yatajikita katika kuutukuza ukweli na wala sio nafasi au cheo cha mtu,  Na ni hatari  wasomi wakifikiri kwamba lengo la vyama vya upinzani ni kushinda viti vya ubunge , madiwani bila kuzingatia maadili na nidhamu basi ni ukweli kuwa hatutakuwa na sababu ya msingi ya kuwaondoa madarakani chama tawala , kwani ugomvi wetu  vyama vya upinzani na chama tawala hausababishwi na tofauti ya rangi za bendera  bali ni msingi katika maadili, nidhamu na uwajibikaji usiozingatia haki na kweli ndio maana kwa sababu hiyo ufisadi,wizi na ubabaishaji umekuwa ukiongezeka kila wakati na kuletea Taifa madhara makubwa.

 Aliyekosa akiwa muungwana anaomba radhi na ndio ushauri wangu kwa David , lakini jambo hili limeshitua lakini pia limefundisha  na jambo la kushangaza hapa,  ni kwanini watu wameshituka sana Mbunge kufutiwa uanachama na sio kwanini Mbunge amekuwa mtovu wa nidhamu  , hata hivyo sifahamu mgogoro huu kwa kina sana , lakini najua  sihitaji ruhusa kuingia chumbani kwangu , mgogoro huu na malumbano yalikuwa wazi tena wazi sana ,

Sasa nimalizie kwa kusema  David bado unayo nafasi kubwa ya kujirekebisha na kuwa kiongozi mzuri , wako waliopata matukio magumu ya kisiasa kuliko wewe lakini waliweza kurudi kwenye nafasi zao kwa utumishi  kama,  Martin Luther King Jr.  alivyopata kunena   “ The ultimate measure of a man is not where he stands in moments of comfort, but where he stands at times of challenge and controversy.

Naibu Katibu mkuu wetu Mh Zitto nimesoma habari mbali mbali kuwa amekukaribisha Chadema ,  lakini mimi kwa sasa  nakukaribisha  Arusha kama utapenda kupumzika huku ukitafakari ili upate kujua kuwa unapaswa kuhama Chama au unapaswa kuomba radhi na kujirekebisha ? Mfano ,ukiuguua ugonjwa wa zinaa pamoja na kutubu dhambi kwa mwenyezi Mungu lakini  pia itakupasa kwenda Hosipatalini kutafuta dawa, sioni kama ni muhimu sana kuhama Chama isipokuwa kuomba radhi hata kama wewe sio Mbunge tena

 “Jipe moyo David Kafulila na Hongera NCCR-MAGEUZI. . Sasa ningekushauri utafute kitabu kinachoitwa  “ THE 21 MOST POWERFUL MINUTES IN A LEADERS DAY “ Kilichoandikwa na na mwandishi maarufu “ John C. Maxwell.

 

If you are a leader , it’s not enough to know what to do . You have to know when to act. “ John C. Maxwell.

Godbless Lema . (Mb)

DJ RAMA ATESA UJERUMANI

Unapotaja orodha ya Ma Dj vijana wa kitanzania ughaibuni jina la Dj Rama,mwenye maskaniyake mjini München ,kule ujerumani ni maarufu kwa kurusha mavitu katika sherehe mbali mbali,Dj Rama amefanikiwa mara nyingi kuwadatisha akili wadau wa muziki kwa kurusha

na kuchanganya muziki wa Tanzania na mingineyo katika sherehe mbali mbali ni juzi tu alikua

mmojawapo wa walio tingisha katika sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania,mjini Berlin

Kutoka Mjengwablog

AFRICA: TUTASAMEHE LAKINI HATUTASAHAU UTUMWA NA BIASHARA YA UTUMWA PERIOD.

New York

Nchi za Afrika zimesema, zinao uungwana wa kutosha kusamehe udhalimu na ukatili wa kutisha ambao waafrika weusi,walifanyiwa kupitia utumwa na biashara ya utumwa.Lakini kamwe hazitaweza kusahau tukio hilo baya kuliko yote katika historia ya mwafrika.

Msimamo huo wa Afrika umetolewa na Mhe. Ombeni Sefue. Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, alipozungumza kwa niaba ya nchi hizo,wakati Baraza Kuu la 66 Umoja wa Mataifai lilipopitisha kwa kauli moja Azimio la Ujenzi wa Mnara wa kudumu wa kumbukumbu ya wahanga wa utumwa na Biashara ya utumwa.

Mnara huo unaotarajiwa kukamilika mwaka 2012 na kugharimu dola za kimarekani milioni 4.5 utajengwa katika eneo maalum hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Tayari mfuko wa ujenzi wa mnara huo umekwisha kuchangiwa zaidi ya dola za kimarekani Milioni Moja na Zabuni kutangazwa.

“Tunapokumbuka na kuadhimisha kumbukumbu ya utumwa na biashara ya utumwa ni lazima pia na kubwa zaidi kutambua na kuheshimu, nguvu, ustahimilivu na moyo wa ushujaa walioonyesha wahanga hao. Walihimili na kuvumilia ukatili wa kila aina, unyanyasaji, uonevu, ubaguzi, mateso, kukandamizwa, kudhalilishwa. Walihamishwa kwa mamilioni katika makazi yao ya asili na kufungwa minyororo na kupelekwa Amerika. Tu waungwana wa kutosha kusamehe lakini kamwe hatutasahu” akasema Balozi Ombeni Sefue.

Akaongeza kwamba, vitendo walivyotendewa watumwa wa asili ya afrika, vitendo vya ubaguzi wa rangi na udhalilishaji, na madhila mengine, bado ni mambo yanayoendelea hadi sasa dhidi ya mwafrika mweusi.

Akasema Afrika inaungana na nchi za visiwa vya Karibian katika kuhakikisha kwamba ujenzi wa mnara wa kudumu wa kumbukumbu ya utumwa na biashara ya utumwa unajengwa na kukamilika kwa kile allichosema mnara huo siyo tu utakuwa ni kuwaenzi watumwa, bali pia utakuwa somo tosha kwa vizazi vya sasa na vijavyo kuhusu historia ya utumwa.

Mwakilishi huyo wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akaongeza pia kwamba, ni jambo la kusikitisha kuona historia ya mtu mweusi na mchango wake katika maendeleo ya ustawi wa mataifa waliokopelekwa haujathaminiwa vya kutosha wala kuwekwa katika machapisho na kumbukumbu nyingineza. Jambo alilozema si sawa na halimtendei haki mwafrika mweuzi.

Na kwa sababu hiyo akahimiza umuhimu na ulazimu wa kuandaliwa kwa machapisho yatakayoonyesha kwa kina nafasi na mchango wa watumwa kutoka Afrika katika maendeleo ya Amerika na nchi nyingine duniani.

Baadhi ya wazungumzaji waliopata nafasi ya kuzungumza wakati wa upitishaji wa azimi hilo, licha ya kutoa michango yao na kuahidi kuendelea kuchangia, walitoa wito kwa nchi ambazo maedeleo yake yametokana na kazi kubwa iliyofanywa na watumwa kujitokeza na kuchangia kwa hali na mali ujenzi wa mnara huo wa kumbukumbu.

Aidha wazungumzaji wengine waliyataka mataifa hayo kuutambua mchango wa watumwa kwa kutoona haya kuomba radhi kwa ukatili mkubwa waliowafanyia binadamu wenzao.

Azimio hilo liliopitishwa pamoja na kuazimia ujenzi wa mnara wa kumbukumbu lakini pia linahimiza kuendeleza kazi ya kuielimisha jamii kuhusu adhari za utumwa na biashara ya utumwa, kuanda machapisho na kuendeleza maadhimisho ya siku ya kimataifa ya utumwa na biashara ya utumwa, maadhisho ambayo hufanyika kila mwaka hapa Umoja wa Mataifa

Swala la Posho Spika Anne Makinda Alichemsha.

Ni dhahiri kauli ya Spika Anne Makinda kuwa wabunge wanaongezewa posho kwa vile gharama ya maisha Dodoma iko juu inaonyesha udhaifu walionao viongozi wetu wengi; kukosa uelewa wa hali halisi.
Kiukweli, kwa kauli ile, Spika Anne Makinda alichemsha.  Na ili tuelewe ni vema tukaingalia picha pana badala ya kipande cha picha. Tatizo hapa si Anne Makinda bali ni mfumo.  Ndio, Anne Makinda ni kielelezo cha tatizo la kimfumo. Kwamba mfumo wetu, mbali ya udhaifu mwingine,  unaowafanya viongozi wetu wawe ’ masultani’. Wakae kwenye nyadhifa za kisiasa na kiserikali  kwa muda mrefu sana kiasi cha kupoteza uelewa wa hali halisi za wananchi wanaowaongoza.
Kwa mfano, tangu niko shule ya msingi nimelisikia jina la Anne Makinda katika nafasi za uongozi.  Hivyo hivyo nimeyasikia majina ya akina Samwel Sitta, Malecela , Pius Msekwa na wengineo. Ndio, ni ukweli, kuwa nchi yetu ambayo asilimia kubwa ina raia vijana inaongozwa na wazee waliostahili kumpumzika na kuwaachia nafasi vijana.
Sina maana kuwa wazee hawana sifa za kuongoza, isipokuwa, tufanye sasa juhudi za makusudi za kuandaa mifumo itakayotufanya nafasi za uongozi zisishikiliwe kwa muda mrefu na watu hao hao. Tuanze sasa kufikiria kwa dhati kuandaa utaratibu wa kuwaandaa vijana ili waje kuwa viongozi bora. Vile vile, utaandae utaratibu  utakaofanya Mbunge asikae bungeni zaidi ya vipindi viwili kwa maana ya miaka kumi.
Angalia sakata hili la wabunge na posho . Kwa hakika ni moja ya mambo ya kuhuzunisha yanayotufungia mwaka. Kwamba imefika mahali wabunge wetu wamefikiria kuongezewa posho kutoka shilingi elfu sabini hadi laki mbili kwa siku, tena katika wakati huu mgumu  kiuchumi ambao mamilioni ya WaTanzania wanaupitia. Huu ni usaliti kwa nchi yetu na si kitu kingine.
Kwa Spika Anne Makinda ,  kama mwanadamu yumkini alighafirika. Ulimi hauna  mfupa na hakuna mwanadamu  asiye katika hatari ya kunena lililo baya masikioni mwa wanadamu wenzake.  Spika Makinda hajachelewa. Atoke sasa, na kwa  sauti yake mwenyewe, awaombe radhi WaTanzania. Akifanya hivyo atasamehewa. Maana atambue, ya kwamba  kuwaambia WaTanzania maisha ya Dodoma kwa Wabunge ni ya gharama ya juu  inatoa tafsiri mbaya.
 Ni kauli mbaya maana Wabunge wetu ukilinganisha na mamilioni ya WaTanzania, hata bila posho ya shilingi hamsini kwa siku, bado watakuwa na maisha ya neema kubwa kuliko wapiga kura wao wengi. Yawezekana kabisa unavyosoma  makala hii kuna mama MTanzania anayejifungua akiwa  amelala sakafuni, au kuna mtoto wa KiTanzania anayekufa kwa malaria kwa vile zahati haina dawa. Ndio hali halisi. Huu ni wakati kwa viongozi wetu kuacha kuendekeza ubinafsi.
Viongozi wakiwamo Wabunge waanze sasa kuwafikiria wananchi ambao wengi wako katika hali mbaya kiuchumi. Ni wananchi hawa ambao miongoni mwao kuna wakulima. Ni wakulima hawa ambao posho ya laki mbili kwa siku kwa mbunge ingetosha kwa mkulima huyu kununua mbolea mifuko mitatu ya kilo hamsini  kwa mfuko. Ni mbolea ya kupandia na kukuzuia kwa ekari moja. Tujiulize; tuko sasa kwenye ” Kilimo Kwanza au Wabunge Kwanza?”

Waziri mkuu mstaafu Cleopa Msuya na Arnold Kilewo Waishambulia serikali kuhusu maendeleo ya kilimanjaro

Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya mkoa wa Kilimanjaro ambaye pia alikuwa Makamu wa Rais na Waziri mkuu mstaafu wa Tanzania Cleopa David Msuya akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani)  kuhusu mkoa wa Kilimanjaro na uendelezaji wa fursa zilizopo kwa maendeleo ya mkoa huo na taifa leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni makamu Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Bw. Arnold Kilewo.
 
Picha na Aron Msigwa -MAELEZO.
 
Na. Aron Msigwa -MAELEZO.

Wananchi wa mkoa Kilimanjaro wametakiwa kutumia fursa zilizopo katika mkoa huo zikiwemo mlima Kilimanjaro, uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro kujiletea maendeleo. Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya mkoa wa Kilimanjaro ambaye pia alikuwa Makamu wa Rais na Waziri mkuu mstaafu wa Tanzania Cleopa David Msuya amesema wananchi wana jukumu la kushirikiana na serikali katika kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo.
Amesema kuwa kwa sasa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimaendeleo licha ya kuwepo fursa nyingi za maendeleo huku akisisitiza kuwa iwapo fursa hizo zitaendelea kutumika ipasavyo wananchi watanufaika na umaskini utapungua. Amefafanua kuwa maendeleo ya mkoa huo yapo wazi kutokana na mkoa huo kuwa na maeneo mazuri ya uwekezaji katika shughuli za kilimo, nguvu kazi na miundombinu mizuri ya kurahisisha ufanyaji kazi.

“Ni dhahiri mkoa wa Kilimanjaro ni moja ya mikoa yenye shule nyingi katika Tanzania, hivyo tuna nafasi nzuri ya kupata maendeleo pamoja na mlima Kilimanjaro tulionao ambao ni kivutio kizuri ndani na nje ya nchi yetu” Amesema. Ameongeza kuwa kwa sasa mlima Kilimanjaro bado haujatumika ipasavyo katika kukuongeza pato la Taifa licha ya mlima huo kuwa na fursa nyingi za kuwainua kiuchumi wananchi hasa katika sekta ya utalii.

Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo wanaoishi maeneo ya mlima Kilimanjaro kuendelea kutunza mazingira yam lima huo ili uendelelee kuwa kivutio cha watalii na kuongeza pato la taifa. Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa jukwaa hilo Bw. Arnold Kilewo amefafanua kuwa kwa sasa jukwaa hilo linaandaa utaratibu wa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo wa mkoa wa Kilimanjaro ili kutathmini na kujadili changamoto mbalimbali za kimaendeleo za mkoa huo na namna ya kuendelea kutumia fursa zilizopo ili kujiletea maendeleo ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda.

 
 

Tuzo aliyopewa Anne makinda ya Lala mikiwa na kupingwa vikali

Kwenye sherehe hizo pamoja na kutunuku Msekwa na Makinda wengi wamejiuliza sababu za kutoswa kwa ‘Spika wa Bunge la Kasi na Viwango’, Samuel Sitta.

Baadhi ya wanasiasa wazoefu waliozungumza na  walisema kuwa wameshangazwa na kitendo cha maspika hao kutunukiwa nishani na Sitta ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kuachwa.

Mmoja wa wanasiasa hao kutoka CCM ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alisema huenda Sitta hakupewa zawadi kutokana na chama hicho tawala kumtuhumu kuwa anaongoza makundi ya upinzani ndani ya chama, jambo ambalo mara kadhaa mwanasiasa huyo amekuwa akilikanusha.

Alisema huenda kutokana na msimamo wake imara usioyumba wa kupambana na vitendo vya ufisadi bila woga ndilo jambo ambalo linalokera wenzake ndani ya chama hicho nakutafsiri kwamba ni kukigawa chama .

Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe alisema hajui vigezo vilivyotumika kutoa nishani hizo lakini yeye anaamini Sitta aliweza kulifanya Bunge kuendesha mambo kiuwazi kiasi cha kuwafanya wananchi wengi kuwa na imani nalo.

“Alisema tangu awali Bunge lake litakuwa la ‘standard and speed’ (kasi na viwango ) na liliweza kuonyesha hilo… lakini mimi Napata kigugumizi cha kusema sababu sijui vigezo vilivyotumika,” alisema Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na alihudhuria sherehe hizo.

Alisema ingawa yeye alichelewa kufika kwenye sherehe hizo, alishangazwa kusikia kuwa Makinda amepata tuzo hiyo wakati kipindi chake cha uspika hakijamalizika.

Spika mwingine ambaye hakutajwa kwenye orodha hiyo ni Yule aliyekuwa wa kwanza baada ya Tanzania kupata uhuru, Chifu Adam Sapi Mkwawa (1964-1973 na 1975-94) na Erasto Mang’enya (1973-75).

Nishani ya juu kabisa iliyotolewa ni ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo walitunukiwa maraisi wa awamu zote tatu zilizopita, Hayati Mwalimu Nyerere ambayo ilipokelewa na Mama Maria Nyerere kwa niaba yake, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.


MY TAKE>
Mtu hutunukiwa nishani based on his or her workdone/accomplished duties sasa huyu speaker wa sasa ndo kwanza ana Mwaka tuu kwenye icho kiti akiboronga in 4 years time atanyanganywa iyo Nishani.
Naona tunaendelea kuuishi ule usemi usemao TZ we are not serious in everything being a reflection of the current regime.